Wanafunzi waliookoka wa makanisa ya Kipentekoste ambao
ni wanachama wa CASFETA-TAYOMI Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) tarehe 19/5/2012 walifanya sherehe
ya kuwaaga wanachama wenzao wanaomaliza masomo yao chuoni hapo, Sherehe hizo zimekuwa za kihistoria kwani idadi ya
wahitimu ilikua kubwa sana ikilinganishwa na miaka mingine kwa mahafali ya Vyuo/Vyuo
vikuu, Wahitimu 270 walitunukiwa vyeti vya CASFETA (CASFETA MEMBERSHIP CERTIFICATES).
Mgeni rasmi katika mahafali hayo alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Dodoma mjini Mheshimiwa
Lephy Benjamin Gembe. Akitoa hotuba yake kwa wahitimu, na wana-CASFETA wote;
Mgeni rasmi aliwaasa vijana hao kuendeleza umoja na mshikamano walionao katika
kuishi maisha ya kumpendeza Mungu ili wawe viongozi bora kwa taifa la Tanzania,
kwa maneno yake mwenyewe alisema “ninyi vijana ndiyo Wakuu wa Wilaya, Wabunge
na Mawaziri wa siku za usoni maana sisi umri umekwenda na tunang’atuka, tutake
tusitake lazima tuondoke na ninyi ndiyo mtachukua nafasi”. Mgeni rasmi
aliipongeza huduma hii ya wanafunzi chini ya TAYOMI kwa kushirikiana na
viongozi wa Serikali hata kuwaalika katika shuhuli za huduma, vilevile aliahidi
kushirikiana na Huduma hii kwa kadri itakavyowezekana.Miongoni mwa wahitimu hao walikuwemo pia Bi. Nancy Ackland ambaye ni Naibu Katibu Mkuu mstaafu wa CASFETA-TAYOMI Tanzania 2010/2011na Bi. Sukama Kameta Mwenyekiti wa Wadada CASFETA-TAYOMI Taifa 2010/2011.
HABARI ZAIDI
KATIKA PICHA
Wana CASFETA Wahitimu wa Chuo Kikuu Cha Dodoma (UDOM) wakiandamana kuelekea Ukumbini kwa akili ya kuanza sherehe rasmi.
Maandamano yameshika kasi huku yakiongozwa na matarumbeta, hii ni Historia haijapata kutokea wahitimu wengi namna hii!!!!!
WanaCASFETA -TAYOMI wahitimu wakiwa wamekaa kwenye nafasi zao huku shughuli za mahafali zikiendelea. Mahafali hayo yalifanyika siku ya Jumamosi 19/05/2012 katika ukumbi wa Happy Cafeteria uliopo chuo cha sayansi ya jamii (College of Social Sciences) katika Chuo kikuu cha Dodoma.
Mwenyekiti mstaafu wa CASFETA-TAYOMI UDOM, Ndugu Matthew Christian (Kushoto) pamoja na Mwenyekiti mstaafu wa Idara ya Wadada CASFETA-TAYOMI Taifa Bi. Sukama Kameta wakiwawakilisha wahitimu wenzao kusoma risala mbele ya mgeni rasmi.
"UTABAKI KUWA MUNGU, UTABAKI KUWA MUNGU, UTABAKI KUWA MUNGU JEHOVA SHAMA!!!" Mgeni rasmi Mheshimiwa Lephy Benjamin Gembe ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Dodoma akiwaongoza makutano kuimba na kucheza wimbo huu wakati wa Mahafali ya CASFETA-TAYOMI Chuo Kikuu Cha Dodoma. Kushoto ni Mwenyekiti wa CASFETA-TAYOMI UDOM.
Mwenyekiti wa CASFETA-TAYOMI UDOM akimlisha mgeni rasmi keki iliyoandaliwa rasmi kwa ajili ya Mahafali, mgeni rasmi alisema kwamba hajawahi kula keki tamu kama hii.